NOVEMBA 23, mwaka huu, viongozi mbalimbai watapewa tuzo za kutambua
mchango wao katika kuboresha afya ya mama na mtoto. 

Tuzo hizo zimeandaliwa na Taasisi ya Madaktari Waliosoma Vyuo Vikuu nchini (THPI), na miongoni watakaopewa tuzo ni Rais Jakaya Kikwete, Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, mke wa Rais, Salma Kikwete na Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi
Kuhusu THPI, ilianzishwa mwezi Machi, 2009 na madaktari 12, na Mkurugenzi  wa taasisi hiyo, Dk. Telesphory Kyaruzi, anasema wanaamini wakiwa wengi, watahudumia watu wengi na jamii kubwa zaidi. Anasema, hadi sasa taasisi ina madaktari  wanachama zaidi ya 120 ambao wamesambaa nchi nzima. "Lengo kuu la taasisi yetu ni kushiriki katika kuhamasisha uboreshaji huduma za afya nchini na kushiriki kikamilifu katika kutoa huduma bora za afya kwa watanzania,"anaongeza. Madaktari hao ni wale walioamua kubaki nchini badalayakukimbilia nje
ya nchi kufanya kazi...kwa kifupi ni madaktari wazalendo.

"Tuliamua kubaki nchini badala ya kwenda nchi za nje kutafuta maslahi mazuri    zaidi kwa sababu ya uzalendo juu ya nchi yetu. "Dira ya taasisi yetu, tunaona watanzania wenye afya bora, huduma bora , na miundombinu bora katika kutoa huduma za afya nchini . Katika taasis yetu  nguvu yetu ni umoja;  wote ni sawa, kila mtu ni muhimu na kila mtu ni kiongozi.  Nguvu yetu ni matumaini,"anaongeza.


 
Dk. Kyaruzi anasema ili kuwa na madaktari wengi sehemu mbalimbali nchini wanaotoa huduma za afya,  taasisi imeanzisha Idara ya Uendelezaji Madaktari Vijana inayoratibu Mtandao wa Madaktari Vijana Nchini, ambao ni Madaktari Wanafunzi( Medical Students), Intern Doctors, na Madaktari wanaoanza kazi ili kuwajengea uwezo    kitaaluma. Aidha, katika kutatua matatizo ya afya nchini, anabainisha kuwa   wanaongozwa na mpango mkakati.



Katika mpango wa mwaka 2011/2014, taasisi imejielekeza katika kutekeleza malengo ya Milenia, lengo la nne na tano, afya ya mama na mototo. Na kufikia lengo la kupunguza vifo vya akina mama kwa 75% ifikapo mwaka 2015. Katika kutekeleza jukumu hili muhimu, taasisi imeanzisha kampeni ya kitaifa ya Saidia Mama Mjamzito Ajifungue salama, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Kutokana na taarifa za jarida la umoja wa mataifa , Global Health and Deplomacy, duniani kina mama  wajawazito 368,000 wanafariki kila mwaka, nafasi ya mama mjamzito kufa ni mara 100 zaidi katika nchi zenye
idadi kubwa ya vifo vya akina mama vinavyotokana na ujauzito. Akifafanua hilo, Dk. Kyaruzi anasema kuwa ni nchi 21 tu duniani ziko kwenye hatua sahihi katika kufikia malengo ya millennia ifikapo mwaka
2015. "Vifo vya mama wajawazito nchini kwa mwaka 2005 vilikuwa ni  578, kwa vizazi       hai 100,000,  na kufikia 454 kwa  vizazi hai 100,000 kwa mwaka 2012.



"Pia vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilikuwa 122 kwa watoto hai 1,000 mwaka 2004 mpaka 81 kwa watoto hai 1,000 mwaka 2012. Na vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja ilikuwa 68 kwa watoto hai 1,000 kwa
mwaka 2004 mpaka 51 kwa watoto hai 1,000 kwa mwaka 2012,"anasema. Kutokana na juhudi kubwa za wadau, anasema wamefanikiwa kumepunguza idadi ya vifo vitokanvyo na ujauzito na vifo vya watoto wachanga,   lakini lazima jitihada za kupunguza vifo vya mama na watoto ziedelee kwa nguvu kubwa zaidi.

Ili kutekeleza kampeni ya Saidia Mama Mjamzito ajifungue Salama, anasema taasisi ilifanya utafiti wa awali,  na kubaini upungufu wa damu ni namba moja, ikifuatiwa na kifafa cha mimba,  Aidha ni asilimia 50 tu ya  wajawazito wanaorudi kujifungua katika vituo vya afya, upungufu wa mindombinu na maambukizi ya Kutoka kwa
mama kwenda kwa mtoto ni changamoto kwa uzazi salama. "Kupitia kampeni tunahamasisha  wananchi kuchangia damu ili kuokoa maisha ya wajawazito wanaohitaji  kwa dharura na kuhamasisha kina baba
kushiriki katika afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na kuwasindikiza  kliniki ili kujua dalili za hatari wakati wa ujauzito na kujiandaa kujifungua.

"Kuongeza uwezo wa miundombinu katika utoaji huduma kwa mama wajawazito ambayo ni matumizi ya simu kufuatilia mama mwenye dalili za hatari kupitia rafiki kliniki mpaka anajifungua salama, kujenga wodi na vyumba vya dharura (ICU) na Upasuaji (Theatres) pamoja na kuzuia maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto,"anaongeza. Akielezea kuhusu tuzo, Dk. Kyaruzi anasema ya Rais Kikwete inatokana   na jitihada mbalimbali, na wanatambua kwa kuipa  kipaumbele sekta ya afya.
Alipoingia madarakani mwaka 2005, bajeti ya sekta ya afya ilikuwa ya  sita, hivi sasa ni ya tatu ikifuatiwa na miundombinu na elimu ambapo sekta hizi zote zinategemeana huku afya ya mama na mtoto ni ya kwanza katika vipaumbele vya Wizara ya Afya. "Rais ameunga mkono kampeni ya malaria haikubaliki ili  kulinda afya ya mama wajawazito na watoto wachanga, katika kufanikisha malengo ya kupunguza vifo vya mama na mtoto duniani, Umoja wa mataifa uliunda tume ya kuratibu taarifa na uwajibikaji juu ya afya ya mama na  mtoto na kumteua Rais Kikwete  kuwa mwenyekiti mwenza  wa tume hii pamoja na Waziri Mkuu wa Canada .
"Hii ni heshima kubwa kwa nchi yetu, ni imani kubwa dunia iliyonayo  juu yetu watanzania. Tuzo hii kwake ni ujumbe kwa jumuia ya kimataifa kwamba na sisi watanzania tunamwamini Rais Wetu,  tunamuunga mkono,"anaongeza. Anaitaja tuzo ya Rais Mstaafu Mwinyi, kwamba imetokana na kazi nzuri
hasa  kupinga maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na jitihada zake za mara kwa mara kuunga
mkono  matembezi ya hisani, kuwezesha upatikanaji wa fedha kusaidia watoto wenye matatizo ya moyo  na saratani ili wapate matibabu ndani na nje ya nchi.


Mkapa naye anapewa tuzo kwa kazi nzuri anayoifanya kupitia taasisi yake ambapo Dk. Kyaruzi anasema, anafana kazi kubwa  kujali afya ya mama na mtoto. Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), nayo ni chanzo kikuu kilichosababisha Mama Salma kupata tuzo kutoka madaktari hao.


Kwa mujibu wadk. Kyaruzi, Mengi anapata tuzo kutokana na utayari wake
kuisaidia jamii,  kupitia vyombo vyake, Taasisi ya Madaktari Wanawake (MEWATA) wamefanya
kazi kubwa ya kuokoa maisha ya wakina mama kutokana na Saratani ya Matiti na Shingo ya
Kizazi. Tuzo za kitaaluma zinaenda kwa Dk. Faraja Nipwapwacha, Daktari  Msaidizi , wa Kituo cha afya Kilimarondo mkoani Lindi , wilaya ya Nachingwea, ambaye kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita hajapata
vifo vinavyotokana na uzazi.

"Uwezo wake wa kujituma na tabia yake ya kufanya  maamuzi sahihi kwa wakati na haraka katika kuokoa maisha ya mama na mtoto, ametoa hamasa kubwa kwamba tunaweza kuzuia vifo vinavyotokana na ujauzito ata sehemu nyingine nchini,"anasema Dk. Kyaruzi.  Anasema THPI inatambua kazi kubwa inayofanywa na wauguzi nchini katika jitihada za kuboresha afya ya mama na mtoto kupitia.

Muuguzi  ambaye amependekezwa na wauguzi wenzake kupitia chama chao  kitaifa cha TANNA ni Elia  Mwumbui kutoka kijiji cha Matongo, kitongoji cha Kimbiji, wilaya ya Ikungi, tarafa ya Ikungi Singida
vijijini kwa kuwa mfano wa wakina baba wanaoshiriki kusindikiza kliniki wake zao wajawazito.

Anasema lengo ni kuhamasisha kuhusu afyaya mama na mtoto, kwani  wanaamini wajawazito na watoto wao wakiwa salama, taifa litakuwa salama na tutajihakikishia ustawi kama Taifa. "Namshukuru  Dk. Mary Nagu, Waziri wa Uwezeshaji na  Uwekezaji  kwa kutuunga mkono, Dk. Asha Rose  Migiro kwa kuwa mlezi wa vijana wa THPI, taasisi na watu binafsi  walioonyesha nia ya kusaidia sehemu ya kampeni hii ya Saidia Mama Mjamzito  ajifungue salama inayoendeshwa na taasisi yetu ya THPI,"anaongeza.


Dk. Kyaruzi anasema wana mradi wa kujenga uwezo kwa vituo vya afya  katika kuzuia maambukizi ya Virusi vya  UKIMWI kutoka kwa mama kwenda  kwa mtoto katika Wilaya za Iringa Vijijini , Wangig'ombe na Mpanda na
umeandaliwa kwa weledi wa hali ya juu na  mshauri mkuu akiwa Dk. David Urassa, unasubiri uwezeshaji wa fedha ili utekelezaji uanze.


"Pia mradi wa ujenzi jengo la akina mama wajawazito kata ya Ikindilo, kituo  cha afya Ikindilo wilaya ya Itilima mkoa mpya wa Simiyu nao unasubiri uwezeshaji wa fedha kuutekeleza,"anamaliza.

Post a Comment

POPULAR POST

 
Top