Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimetangaza kuongeza viwango vya ada za masomo na malazi kuanzia mwaka ujao wa masomo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyeki wa Baraza la Udom, Balozi, Dk. Juma Mwapachu, alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya Nne ya chuo hicho yaliyofanyika mjini hapa.
Balozi Mwapachu alisema lengo la chuo hicho kuongeza ada ni kukiwezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wanafunzi hao.
”Uamuzi huu unatokana na kupanda kwa gharama za uendeshaji pamoja na ufinyu wa bajeti kutoka serikalini…hata hivyo ieleweke kwamba chuo chetu bado kitakuwa kinatoza ada na gharama ya malazi kwa viwango vya chini kulingana na vyuo vingine vya kiserikali,” alisema.
NIPASHE ilipotaka kujua ni kiwango gani cha ada kitaongezwa, Afisa Uhusiano wa Udom, Beatrice Bartazar, alisema suala hilo bado halijapitishwa rasmi kwani hiyo ni mipango ya mwakani.
Alisema suala hilo linatarajiwa kujadiliwa kwenye vikao kwanza ndipo kitapatikana kiwango halisi kitakachoongezwa.
Naye, Makamo Mkuu wa Chuo cha Udom, Profesa Idris Kikula, alisema ujenzi wa Kituo cha Uchunguzi wa Afya kinachogharamiwa na Mfuko wa Afya wa Bima (NHIF) kimekamilika kwa asilimia 96.
Profesa Kikula alisema kituo hicho kinatarajiwa kufunguliwa rasmi hivi karibuni na Rais, Jakaya Kikwete.
”Tunasubiri ununuzi wa vifaa na samani kabla ya shughuli hiyo kufanyika,” alisema
Pia, alisema NHIF inatarajia kujenga hospitali kwa ajili ya kufundishia wanafunzi ambapo ujenzi huo unatarajia kufanyika hivi karibuni.
”Kituo na hospitali hiyo vitatoa msaada mkubwa kwa wanafunzi wa Chuo cha Sayansi za Afya kwa kuwawezesha kupata uelewa mkubwa katika masomo yao,” alisema
Katika mafahari hayo, mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa ambaye aliwatunuku vyeti watahiniwa 5,218.