VYAKULA VINAVYOONDOA MAUMIVU WAKATI WA HEDHI KWA WANAWAKE.
KILA mwanamke hupitia hatua ya kupatwa na hedhi mara moja kwa mwezi,
ikiwa ni maumbile ya kawaida waliyoumbwa nayo. Lakini wanawake wengi
husumbuliwa na matatizo kadhaa siku chache kabla au wakati wa siku zao,
matatizo hayo hutofautiana kati ya mtu na mtu kutegemeana na afya ya
muhusika.
DALILI ZA MATATIZO YA HEDHI
Siku chache kabla ya hedhi, baadhi ya wanawake hupatwa na hofu na huwa
wenye hasira. Husumbuliwa na mfadhaiko wa akili, huumwa na kichwa,
matiti hujaa maziwa, hukosa usingizi na kuvimba sehemu za siri. Hali hii
husababishwa na kukosekana kwa uwiano wa homoni (Homone imbalance) na
hali hii huweza kukoma ndani ya saa 24 baada ya kuanza hedhi.
MAUMIVU MAKALI YA HEDHI
Wengine hupatwa na maumivu makali sana wakati wa hedhi. Maumivu hayo
huwapata akina mama ama siku mbili ama tatu kabla au mara tu waanzapo
siku zao. Hali hii pia inasababishwa na kutokuwepo kwa uwiano wa homoni
mwilini, ambako kumesababishwa na ukosefu wa virutubisho fulani.
Wengine hutokwa na damu nyingi kuliko kawaida au kukaa katika siku za
hedhi kwa kipindi kirefu kuliko kawaida. Kuna sababu nyingi zinazoweza
kuchangia hali hii, ikiwemo kuugua kwa muda mrefu, kupatwa na hofu,
huzuni, mshtuko na sababu nyingine za kitabibu.
JUISI YA MBOGA ZIFUATAZO HUTIBU
Kwa kutumia vyakula asilia unaweza kuepukana na maumivu ya mara kwa mara
wakati wa siku zako. Katika orodha ndefu ya juisi za mboga zinazotibu
kwa uhakika matatizo yote ya hedhi, ni Kotimiri (Parsley), mboga ya
majani ambayo upatikanaji wake ni rahisi. Kwa mujibu wa watafiti,
Kotimiri ina uwezo wa kurekebisha uwiano wa homoni hivyo kuondoa
matatizo kadhaa ya hedhi.
Inaelezwa kuwa uwezo wa Kotimiri kurekebisha matatizo ya hedhi unatokana
na kuwa na aina ya kirutubisho kiitwacho ‘Apiol’ ambacho pia kimo
miongoni mwa homoni za jinsia ya kike (estrogen). Maumivu na mvurugiko
wa siku hurejea katika hali ya kawaida kwa kunywa juisi ya Kotimiri mara
kwa mara.
Aidha, juisi hiyo inapochanganywa na juisi ya viazi pori (Beet Root),
karoti au matango huwa na nguvu zaidi. Kiwango kinachoshauriwa
kuchanganya kiwe na ujazo sawa kwa kila aina ya juisi utakayochanganya.
Juisi yenye mchanganyiko huo ni rahisi kutengeneza na ni dawa inayoweza
kumsaidia mwanamke wakati wote wa maisha yake bila kuhitaji kutumia dawa
zingine kali za kuzuia maumivu (pain killers) ambazo huwa na madhara
baadaye.
TANGAWIZI NAYO HUTIBU
Tangawizi nayo ni dawa nzuri sana ya kutibu matatizo yatokanayo na
hedhi, hasa katika tatizo la maumivu makali na kutokupata hedhi. Chukua
kipande cha tangawizi mbichi, kiponde na kiweke kwenye kikombe cha maji
ya moto kwa dakika chache, kisha tia sukari kiasi na unywe mchanganyiko
huo, kwa siku mara mbili kila baada ya mlo.
UFUTA NAO NI DAWA
Ufuta (Sesame) nao ni miongoni mwa mbegu za asili unazoweza kula na
kutibu matatizo ya hedhi. Saga ufuta na pata unga wake kisha uchanganye
na maji ya moto, kunywa mara mbili kwa siku. Kinywaji hiki huondoa
maumivu wakati wa hedhi kwa wasichana wadogo.
Ukitumia mara kwa mara kinywaji hiki cha ufuta, hutibu pia tatizo la
kupata hedhi kidogo. Pia unaweza kuchangaya maji ya kuoga ya uvuguvugu
na mbegu za ufuta zilizopondwa pondwa kiasi cha kiganja kimoja, nayo
hutoa nafuu kubwa kwa wanaosumbuliwa na maumivu, hasa ukitumia siku
mbili kabla ya siku zako.
PAPAI NALO NI DAWA
Mungu ametuumba na kutupa mazao mengi ambayo yana uwezo wa kutatua
matatizo yetu ya kiafya, iwapo tutagundua siri hiyo. Papai bichi nalo
linaelezwa na watafiti wetu kuwa lina uwezo wa kulainisha misuli ya njia
ya uzazi hivyo kufanya utokaji wa hedhi kuwa mwepesi usio na maumivu.
Papai huwa na manufaa zaidi kwa wasichana haswa kwa wale wenye tatizo la
kutopata siku zao kutokana na kuwa na ‘stress’ au mawazo. Utapata faida
hiyo kwa kula mara kwa mara tunda hilo bichi (ambalo halijaiva lakini
limekomaa)