MAAJABU YA KARANGA
Wengi wetu huchukulia ulaji wa karanga kama
chakula cha kujiburudisha na kisichokuwa na
umuhimu sana katika afya ya mwili wa binadamu.
Kiukweli karanga siyo chakula cha kupuuziwa
iwapo utajua faida zake kama nitakavyokujuza leo
katika makala haya.

MAGONJWA YA MOYO….
Kama ilivyokuwa kwa korosho, karanga nazo ni
chanzo kizuri cha mafuta mazuri aina ya
‘monounsaturated fats’ ambayo yanatiliwa mkazo
kutumiwa kwa afya ya moyo. Kwa mujibu wa
utafiti, watu wanaokula karanga mara kwa mara
hupunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa
moyo (cardiovascular heart disease) kwa asilimia
21.

Aidha, katika taarifa iliyochapishwa kwenye jarida
moja la Uingereza la ‘Journal of Nutrition’
ambako kuna matokeo ya taarifa nne za utafiti,
imeonesha pia watu wanaotumia karanga mara

kwa mara, angalau mara nne kwa wiki, hujipa
kinga nyingine dhidi ya ugonjwa wa moyo
(coronary heart disease) kwa zaidi ya asilimia 37.

Mbali ya kuwa na mafuta mazuri yanayotoa kinga
kwenye moyo, karanga pia, hasa za kukaanga,
zinaelezwa kuwa na kiwango kikubwa cha
virutubisho vinavyotoa kinga ya mwili
(antioxidants) kuliko hata kile kinachopatikana
kwenye tunda la epo na karoti!

Ili kupata kinga hiyo dhidi ya aina hizo mbili za
ugonjwa wa moyo, ambao unatesa watu wengi
duniani na kugharimu pesa nyingi kwa matibabu,
unashauriwa kula karanga pamoja na bidhaa zake
kama vile ‘peanut butter’, angalau kijiko kimoja
cha chakula, mara nne kwa wiki.

KINGA DHIDI YA KIHARUSI……
Ugonjwa mwingine hatari unaosumbua watu
wengi hivi sasa ni kiharusi au ‘stroke’, lakini
unaweza kujikinga nao kwa kuwa na mazoea ya
kula karanga tu.

Utafiti umeonesha kuwa karanga ina kirutubisho
aina ya ‘Resveratrol’ ambacho hupatikana pia
kwenye zabibu na mvinyo mwekundu (red wine).
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa maabara na

kuchapishwa kwenye jarida la Kilimo na Kemia ya
Chakula (Journal of Agricultural Food Chemistry),
umeonesha kuwa kirutubisho hicho huimarisha
utembeaji wa damu kwenye mishipa inayokwenda
kwenye ubongo kwa kiasi cha asilimia 30.

KINGA DHIDI YA KANSA YA TUMBO….
Faida nyingine inayoweza kupatikana kwenye
mwili kutokana na ulaji wa karanga, ni kinga dhidi
ya ugonjwa wa saratani ya tumbo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa, unaonesha
kuwa virutubisho vya ‘folic acid’, ‘phytosterols’,
‘phytic acid’ (inositol hexaphosphate) na
resveratrol’ vinavyopatikana kwenye karanga,
huweza kutoa kinga dhidi ya ugonjwa wa saratani
ya tumbo.

Zaidi utafiti huo umeonesha kuwa ulaji wa
karanga, hata mara mbili tu kwa wiki, una uwezo
wa kupunguza uwezekano wa kupatwa na saratani
ya tumbo kwa asilimia 58 kwa wanawake na
asilimia 27 kwa wanaume!

Kwa maelezo hayo kuhusu faida za karanga
mwilini, bila shaka chakula hiki kinapaswa kupewa
kipaumbele katika orodha ya vyakula tunavyokula
kila siku na hakika Mungu ametupenda sana kwa
kutupa kinga dhidi ya maradhi yote yanayotukabili
kwa njia ya vyakula.

Post a Comment

POPULAR POST

 
Top