Ikifika mahali mtoto mdogo anasema anawakumbuka wazazi wake kwa sababu ya mateso anayoyapata ugenini ujue ni zaidi ya ukatili, tena ni ukatili wa kutisha.
Watoto hao, kwa sasa wanaishi Nzasa ‘A’, Kata ya Charambe, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na ndiko walikopatia mateso yote.
MAMBO YALIPOANZA KUTIBUKA
Wiki iliyopita, watoto hao waliokolewa na majirani katika kifungo cha miezi sita ndani huku afya zao zikiwa zimedhoofu kwa kukosa chakula.
Ilidaiwa kwamba, watoto hao Hassan na Hussein ambao ni mapacha na Rehema, walifungiwa katika banda la shangazi yao aitwaye Asia Bora ambalo ujenzi wake haujakamilika. Wamekuwa wakiishi humo kwa kula mabaki ya vyakula jalalani.
USHUHUDA WA MAJIRANI
Wakizungumza na gazeti hili hivi karibuni, majirani wa nyumba hiyo walimweleza mwandishi wetu kuwa watoto hao wamekuwa wakionekana nje ya nyumba hiyo mara chache sana wakiwa wanagombania mabaki ya vyakula kwenye jalala.
“Tumekuwa tukiwaona nje mara chache kwenye jalala. Unajua, Asia (shangazi yao) aliwachukua kwa kaka yake, Kijiji cha Namakongoro Kata ya Lihimalyao huko Kilwa mkoani Lindi.
“Tukasikia lengo lake aje kuishi nao kwa vile yeye Mungu hamkujalia kupata watoto. Lakini maisha hapo kwake yakawa siyo mazuri kwa kipato kwa mama huyo.
Mmoja wa majirani hao aliyejitambulisha kwa jina la Aisha Ramadhan yeye alikwenda mbele zaidi kwa kusema:
“Hapo awali tulikuwa tukiwaona wakitoka nje na kucheza na watoto wetu huku wakiwa na afya nzuri. Asia akatueleza kuwa ni watoto wa nduguye, amewachukua huko kijijini.
“Baada ya muda fulani tukawa hatuwaoni, tulidhani amawarudisha kwao, lakini kadiri siku zilivyokuwa zinakwenda mbele tukawa tunawaona mara chache wakiwa jalalani wanapigania mabaki ya chakula.
“Kuna siku mimi niliwakamata wakiwa wamebeba mfuko wa rambo wenye kinyesi, walikuwa wanakuja kutupa katika maeneo yetu, nikawarudisha nao kwa shangazi yao. Kumbe nyumba wanayoishi haina choo ndiyo maana wamekuwa wakijisaidia kwenye rambo.
“Siku moja walipotoka nje kutafuta chakula jalalani, mimi na majirani wenzangu tuliwauliza wanaishije? Wakatuambia hawapewi chakula na shangazi yao akitoka asubuhi harudi mapema, akirudi inakuwa ni usiku sana wao wakiwa wameshalala.
“Inasikitisha sana kuwaona watoto hawa wanaachwa peke yao kutwa nzima bila mtu wa kukaa nao na wamekuwa wakifungiwa ndani kwa muda mrefu sasa, ila huwa wanakiuka masharti na kutoka kwa ajili ya kutafuta mabaki ya chakula.
Jirani huyo akaendelea kuanika mateso ya watoto hao: “Kwa kuwaonea huruma tumekuwa tukilazimika kuwapa chakula, lakini Asia anaporudi na kugundua hilo anawapiga, kwa hiyo wakawa waoga kuja kuchukua chakula. Mimi niliumia hadi machozi.”
Jirani: “Baadaye wakawa hawaonekani, lakini cha ajabu mara nyingi tukiamka asubuhi tunakuta mifuko ya rambo yenye vinyesi imetapakaa, tukimweleza Asia inakuwa ugomvi.
“Siku moja baada ya shangazi yao kuondoka, nilikwenda kuwachungulia ndani, nikawaona wamekonda sana, wamepauka na wamevaa nguo zilizochakaa.
“Nilitokwa machozi, nililazimika kuwaita wenzangu nao walipofika hakuna aliyejizuia kulia. Tukasema hawa watoto watakufa, ndiyo tukaamua kuwaokoa kwa kupeleka taarifa kwa mzee Dadi Salum ambaye ni polisi jamii wa hapa.
POLISI JAMII NAYE ALIA
“Mzee Dadi naye alipofika na kuwaona kwa macho alilia, watu wakaanza kukusanyika, tukawatoa nje watoto, kila mmoja aliwaonea huruma. Tuliwachukua hadi Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Nzasa A.
SHANGAZI MTU ANUSURUKA KIPIGO
“Hatujui ni nani aliyempigia simu Asia, kwani muda mfupi tu tukasikia yupo nyumbani kwake. Uongozi wa mtaa ulimfuata, walipofika, wanawake wenzake hasa wale anaochukua nao mkopo wa fedha benki walitaka kumpiga wakimuuliza pesa anapeleka wapi.
“Hata hivyo aliokolewa na polisi jamii ambao walimchukua na kumweka katika Bajaj na kumpeleka Kituo cha Polisi Mbagala kwenye Dawati la Jinsia na Watoto, watoto nao pia walipelekwa huko.”
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nzasa A, Mrisho Salum alikiri kuwapokea watoto hao wakiwa katika hali mbaya kiafya, wakapelekwa polisi. Akawataka wananchi kutokaa kimya mara wanapoona vitendo kama hivyo.
Mwandishi alifika hadi kituo cha polisi na kuambiwa na askari mmoja kuwa mapacha walichukuliwa na mtu aliyejitambulisha kwa jina la Othman Mbwana aliyedai ni babu yao.
Mbwana alidai kwamba ameamua kuwachukua watoto hao wakaishi nyumbani kwake wakati akifanya mawasiliano na wazazi wao.
“Kwanza nitawapeleka hospitali wakatazamwe afya zao, ila nimesikitishwa sana na hali hii, sijajua ni kwa nini watoto hawa wamefikia hatua hii,” alisema Mbwana.
Rehema yeye alichukuliwa na mjomba wake aitwaye Sood Ismail ambaye alidai anakwenda kukaa naye hadi hapo atakapofanya mawasiliano na wazazi wa huyo mtoto, akisema kitendo cha Asia kimeidhalilisha familia.
RPC TEMEKE ATUPIA NENO
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo amewataka wananchi kufichua vitendo viovu ndani ya jamii na amewapongeza vijana wake wa ulinzi shirikishi kuokoa maisha ya hao watoto.
Post a Comment