Lakini pamoja na faida zote tunazozipata, ukweli unabaki palepale kwamba pombe ina athari katika maisha ya binadamu.
Mwanzoni mwa mwaka huu wataalamu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na madaktari wastaafu walikutana na wanahabari jijini Dar es Salaam na kuzungumzia juu ya mkutano utakaozungumzia athari za pombe katika jamii.
Mkutano huo unaotarajia kufanyika Jan 13 hadi 14 mwaka huu mkoani Arusha, utashirikisha nchi za Afrika Mashariki.
Watunga sheria na wataalamu wengine kutoka serikalini watahudhuria huku ujumbe wa mkutano huo ni: ‘Kilevi si bidhaa ya kawaida na ni kikwazo katika maendeleo.’
Mkurugenzi Msaidizi na Katibu wa Magonjwa yasiyoambukiza, Dk. Joseph Mbatia, kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii anasema serikali ipo mbioni kutengeneza sera itakayohusu utumiaji wa pombe ili kupunguza athari zake katika jamii.
Dk. Mbatia anasema wamelazimika kutunga sera hizo baada ya kuona matatizo yanayotokana na pombe yanaongezeka kila kukicha.
Anasema kabla ya sera hizo kupitishwa watafanya utafiti katika maeneo mbalimbali ili kujua ni jinsi gani jamii inavyolichukulia suala la pombe na madhara yake.
“Mfano, katika vijiji vichache tulivyofanya utafiti, wananchi walikuwa wakijitetea kwamba pombe imewasaidia kuendesha maisha yao…lakini ukweli ni kwamba pamoja na faida ambazo zimekuwa zikiorodheshwa, hasara ni nyingi kuliko faida.
“Kwa mfano, bima zimekuwa zikilipwa kutokana na ajali zinazosababishwa na kulewa kupita kiasi,” anasema Dk. Mbatia.
Anabainisha kwamba sera zitakazowekwa si katika kupiga vita biashara ya pombe na badala yake zitakuwa zikiangalia njia bora za matumizi yake na kwa wale wataoonekana wameshaathirika watawekewa utaratibu wa kupatiwa tiba.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kanda ya Afrika Mashariki ya ‘IOGT-NTO Movement’, ambao ni waandaaji wa mkutano huo, Gunnar Lundstrom, anasema bado kuna changamoto zinazolikabili taifa katika kupunguza athari za pombe.
Anasema changamoto hizo ni pamoja na pombe kupatikana kwa gharama nafuu na hivyo kusababisha watu kunywa kupindukia.
Tatizo lingine anasema ni pombe kuwa moja ya chanzo cha mapato nchini, jambo linalofanya serikali kushindwa kupiga marufuku.
Naye Daktari mstaafu, Maletnlema Tumsifu, anasema kuna jumla ya magonjwa 60 yanayosababishwa na unywaji wa pombe.
Anataja baadhi ya magonjwa hayo kuwa ni mfarakano katika familia, maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi, unene kupita kiasi, utapiamlo hasi, mimba kuharibika na kisukari.
Dk. Maletnlema anasema kuna madhara ya pombe ya aina mbili. Kwanza ni kuathirika kwaa mishipa ya fahamu mwilini kote kwa kupunguzwa uwezo na pili ni kuungua baadhi ya ogani za mwili hasa tumbo pindi mtu anapokunywa.
Anaeleza kwamba katika kuathirika mishipa ya fahamu kumetizamwa kwa hatua nne za wanywaji, hatua ya kwanza ni ile ya kuchangamka.
Hapa mtu hujisikia mzima zaidi ya kawaida, moyo unapiga haraka, tumbo linameng’enya chakula haraka na hamu ya chakula kuongezeka.
Hatua ya pili, mtu akiendelea kunywa anachanganyikiwa na kuzungumza sana, kukosa aibu, utu kubadilika, kutawala tabia za kimwili, hamu ya chakula kuongezeka na hapa ndipo watu wanaagiza nyama choma kwa wingi.
Mnywaji akiendelea kunywa pombe hucharuka kutokana na neva zake za ubongo kushindwa kumiliki mwili.
Mambo yote anayoyafanya hayana utaratibu kwani mnywaji huwa mkorofi.
Dk. huyo anasema mnywaji huwa mkorofi na anaongea maneno yasiyo na maana, baadhi ya wanywaji huchukulia hatua hii kama raha yao. Hapa kitu kinachojitokeza ni kupoteza hamu ya kula.
Hatua ya nne mtu akilewa kupita kiasi huwa hajijui na analala fofofo kutokana na kupoteza fahamu. Huenda akajikojolea au kutapika, inategemea na kiasi cha pombe alichokunywa.
Wakati kwa upande wa ogani, pombe huathiri zaidi viungo vinavyopata pombe nyingi kila wakati mtu akiwa anakunywa.
Mfano wa viungo hivyo ni mdomo, koo na tumbo, ambavyo vyenyewe hufikiwa na pombe nyingi mara mtu anapomeza.
Tumbo likiumia inaonekana kama maumivu ya tumbo, pengine kutapika na kuharisha. Lakini kutokana na utaratibu wa tumboni, lazima chakula chote pamoja na sumu au madawa vinavyonyonywa tumboni vipitie katika ini kuondoa sumu na vyakula visivyohitajika.
Na kwa sababu hii, pombe yote mtu anayokunywa hupita katika seli za ini na zinajaribu kuiondoa lakini nazo zinalewa chakari na baadhi zina kufa.
Ieleweke kwamba tukinywa kidogo seli chache zinakufa na tukinywa sana zinakufa seli nyingi na nafasi yake inajazwa nyuzi nyuzi za kovu.
Ini huwa na mabilioni ya seli ambazo ni imara, hata mtu akinywa pombe nusu, seli zake bado zitaendelea na maisha kama inafikia kikomo ini linashindwa kufanya kazi na kujikuta njia za nyongo na mishipa ya damu inaziba.
Kila ogani ya mwili inaumia kivyake, lakini tumbo na ini ni mifano wazi.
Post a Comment