Tarehe 11 Oktoba 2013, Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO)
liliwasilisha maombi ya kurekebisha
bei ya umeme kwa Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na
Maji (EWURA). TANESCO
ilipendekeza kuongeza bei kwa
asilimia 67.87 kuanzia tarehe 1
Oktoba 2013, asilimia 12.74 kuanzia
tarehe 1 Januari 2014 na asilimia 9.17
kuanzia tarehe 1 Januari 2015.
Vilevile TANESCO waliomba
kuidhinishwa kwa kanuni ya
kurekebisha bei ya umeme kulingana
na mabadiliko ya bei za mafuta,
mfumuko wa bei na mabadiliko ya
thamani ya shilingi ya kitanzania.
Aidha, TANESCO iliomba
kuidhinishwa viwango vya gharama
za kuunganisha umeme
vinavyozingatia ruzuku
inaliyotolewa na Serikali, na
kuidhinishwa tozo mbalimbali kwa
huduma zitolewazo na TANESCO.
Kwa mujibu wa TANESCO,
kupitishwa kwa maombi haya
kutaliwezesha Shirika (a) kupata
fedha za uendeshaji na uwekezaji wa
miundombinu, (b) kulifanya Shirika
liweze kukopesheka na hivyo
kuwezesha kupata mikopo yenye
masharti nafuu, (c) kuliwezesha
Shirika kukabiliana na ongezeko la
mahitaji ya umeme kwenye Gridi ya
Taifa, na (d) kuongeza uwezo wa
kufanya matengenezo ya mara kwa
mara ya miundombinu iliyopo ili
kuhakikisha kunakuwa na
upatikanaji wa huduma za umeme
wa uhakika kwa wateja.
Itakumbukwa kwamba bei za umeme
zinazotumika hivi sasa ziliidhinishwa
mwezi Januari 2012. Bei hizo
zilipanda kwa asilimia 40.29
ikilinganishwa na maombi ya
TANESCO ambapo ilipendekeza bei
zipande kwa wastani wa asilimia
155. Sababu ilikuwa ni kuongezeka
kwa gharama za uendeshaji
kulikosababishwa na hali ya ukame
katika maeneo yanayotiririsha maji
katika mabwawa ya kuzalishia
umeme, toka mwaka 2011. Hali hiyo
ilipelekea TANESCO kulazimika
kununua umeme kwa gharama
kutoka kwa wazalishaji wa dharura
(Emergency Power Producers). Hali
ya maji katika mabwawa ya
kuzalishia umeme bado sio nzuri na
hivyo TANESCO itaendelea kununua
umeme kutoka kwa wazalishaji wa
dharura (Emergency Power
Producers).
USHIRIKISHWAJI WA WADAU
Kulingana na Kifungu Na. 19(2) (h)
cha Sheria ya EWURA, Mamlaka
ilifanya Taftishi ili kupata maoni juu
ya ombi la kurekebisha bei za
umeme. Ukusanyaji wa maoni
ulihusisha pia mikutano minne (4)
iliyofanyika Iringa na Shinyanga
tarehe 15 Novemba 2013, Bagamoyo
tarehe 20 Novemba na kuhitimishwa
Dar es Salaam tarehe 22 Novemba
2013. Aidha, tarehe 6 Desemba 2013,
EWURA iliitisha mkutano wa mwisho
wa wadau wakiwemo wawakilishi
kutoka Wizara ya Nishati na Madini
(MEM), TANESCO, Shirika la Umeme
la Zanzibar (ZECO), Shirikisho la
Wenye Viwanda Tanzania, Baraza la
Watumiaji na Baraza la Ushauri la
Serikali, Umoja wa Wazalishaji wa
Saruji wa Afrika Mashariki, na
kiwanda cha ALAF. Katika mkutano
huo EWURA iliwasilisha mwelekeo
wa maamuzi kuhusu maombi ya
TANESCO na namna
zilivyokokotolewa. Wadau walipewa
fursa ya kutoa maoni yao kuhusu
mwelekeo wa bei na maoni yao
yamezingatiwa katika kufikia
maamuzi ya mwisho.
UCHAMBUZI NA UAMUZI
Kwa kufuata sheria na kanuni
zinazoelekeza kuhusu uchambuzi wa
bei ya umeme, EWURA ilifanya
uchambuzi wa kifedha na kiufundi ili
kubaini uwezo wa TANESCO katika
kutekeleza majukumu yake ya kila
siku. Uchambuzi uliangalia utendaji
wa Shirika la TANESCO katika miaka
iliyopita na pia iliangalia majukumu
yanayoikabili TANESCO katika miaka
mitatu ijayo. EWURA imebaini
kwamba hali ya kifedha ya Shirika la
Umeme sio nzuri. Shirika limeendelea
kupata hasara, ambayo iliongezeka
kutoka shilingi bilioni 47.3 katika
mwaka 2010 na kufikia shilingi bilioni
223.4 mwishoni mwa mwaka 2012.
Pamoja na mapungufu ya kiufanisi,
sababu kubwa ya ongezeko la hasara
ni kuongezeka kwa gharama za
uzalishaji wa umeme ambao
TANESCO inanunua kutoka kwa
wazalishaji binafsi. Hali hii
imelifanya shirika kushindwa kulipa
madeni yake ya muda mfupi na ya
muda mrefu, ambayo yamelibikizwa
na kufikia TZS 456.8 bilioni tarehe 22
Novemba 2013, hali ambayo inatishia
uendelevu wa huduma ya umeme
hapa nchini.
Mamlaka imetumia Kanuni ya
Ukokotoaji wa Bei kama
ilivyopendekezwa na AF-MERCADOS
wakati wa kukokotoa mahitaji ya
mapato ya TANESCO. Kanuni hiyo
inawezesha kukokotoa bei
zinazolandana na gharama halisi
kwenye mfumo wa umeme na
kuzigawa kwenye makundi ya
watumiaji umeme, kadiri kila kundi
linavyosababisha gharama kwenye
mfumo wa umeme kwa mujibu wa
mahitaji ya Sheria ya Umeme ya 2008
Kifungu cha 23(2)(f).
EWURA imejiridhisha kwamba,
ufumbuzi wa matatizo ya kifedha ya
TANESCO, unahitaji njia/mikakati
miwili itekelezwe kwa pamoja:
kuongeza bei ya umeme ili kufikia bei
inayokidhi gharama halisi (Cost
Reflective Tariff); na
TANESCO kupata mkopo wa
gharama nafuu ama ruzuku kutoka
Serikalini ili kulipa limbikizo la
madeni ya Shirika.
Bodi ya Wakurugenzi wa EWURA,
katika kikao chake cha tarehe 10
Desemba 2013 pamoja na mambo
mengine, ilitoa maamuzi ya ongezeko
la bei za umeme kwa viwango
mbalimbali kwa makundi mbalimbali
ya wateja, kama ifuatavyo:
Kundi D1: Hili ni kundi la wateja
wadogo wa majumbani, hasa vijijini,
ambao hutumia wastani usiozidi wa
Uniti 75 kwa mwezi. EWURA
imeongeza wigo wa mahitaji ya
umeme na kufikia uniti 75 kwa
mwezi, lengo likiwa ni kuongeza
idadi ya wateja wa TANESCO
wanaoweza kulipa kidogo kwa
matumizi ya umeme kwa kiwango
hicho, na pia kuwahamasisha
kutumie zaidi umeme. Awali kundi
hili lilikuwa linatunia wastani wa
matumizi ya uniti 50 kwa mwezi. Bei
mpya ni shilingi 100 kwa uniti moja,
kutoka shilingi 60 za sasa, sawa na
ongezeko la shilingi 40.
Kundi T1: Hili ni kundi la watumiaji
wakubwa wa umeme majumbani,
biashara ndogondogo, mashine za
kukoboa na kusaga nafaka, taa za
barabarani, mabango n.k. Bei
iliyoidhinishwa ni shilingi 306 kwa
uniti moja, ikiwa ni ongezeko la
Shilingi 85 ya bei ya sasa. TANESCO
ilipendekeza ongezeko la shilingi 131.
Kundi T2: Hili ni kundi la watumiaji
umeme wa kawaida ambao hupimwa
katika msongo wa volti 400, na
ambao matumizi yao ya wastani kwa
mwezi ni zaidi ya uniti 7,500 wateja
wafanyabiashara kubwa, viwanda
vya kati. Bei ya nishati iliyoridhiwa
ni shilingi 205 kwa uniti moja, sawa
na ongezeko la shilingi 73 ya bei ya
sasa. TANESCO walipendekeza
ongezeko la shilingi 145 ya bei ya
sasa.
Kundi T3-MV: Hili ni kundi la wateja
wakubwa kama viwanda vikubwa
waliounganishwa katika msongo wa
kati (Medium Voltage). EWURA
imeidhinisha bei ya nishati kwa
kiwango cha shilingi 166 kwa uniti
moja, sawa na ongezeko la shilingi 45
ya bei ya sasa. TANESCO
walipendekeza ongezeko la shilingi
148 kwa uniti moja.
Kundi T3-HV: Hili ni kundi la wateja
wakubwa waliounganishwa katika
msongo wa juu (High Voltage – Voti
66,000 na zaidi) ikiwa ni pamoja na
ZECO, Bulyanhulu, na Twiga Cement.
Bei iliyoidhinishwa ni shilingi 159
kwa uniti moja, sawa na ongezeko la
shilingi 53 la bei ya sasa. TANESCO
waliomba ongezeko la shilingi 80 kwa
uniti moja.
Bei ya umeme itakuwa inarekebishwa
kila baada ya miezi mitatu kulingana
na mabadiliko ya kiwango na bei za
mafuta; mfumuko wa bei, mabadiliko
ya thamani ya fedha, na upatikanaji
wa ruzuku toka Serikalini.
Vilevile, TANESCO inatakiwa
kutekeleza miradi ya uwekezaji
iliyoainishwa kwa kutumia fedha
zitakazokusanywa kutokana na bei
zilizoidhinishwa. EWURA inaweza
kurekebisha bei ya umeme ya
TANESCO kila mwisho wa mwaka
2014 na/au mwaka 2015 endapo
TANESCO itashindwa kutekeleza
miradi iliyotajwa katika Jedwali
husika. Marekebisho hayo
yatatokana na makadirio ya
gharama za miradi ambayo
haikutekelezwa.
Kutokana na matazamio ya kuwa na
mabadiliko makubwa katika
uzalishaji wa umeme (generation
mix) katika mwaka 2015 na
kuendelea, kutokana na matarajio ya
kuongezeka kwa kwa upatikanaji wa
gesi asilia, EWURA itafanya utafiti
kubaini gharama halisi (Cost of
Service Study) ya huduma ya umeme
kwa wakati huo. Hivyo, bei
zilizoidhinishwa zitatumika mpaka
mwaka 2016, kama utafiti
unaotazamiwa kufanywa
hautakamilika kabla ya mwisho wa
mwaka 2015.
EWURA ililinganisha bei za umeme
kwa kila Uniti, katika nchi za Afrika
ya Mashariki, na kuona kuwa bado
bei za umeme za Tanzania zipo chini
ukilinganisha na bei za katika nchi
jirani kama inavyoonyeshwa hapa
chini, kwa makundi mbalimbali ya
watumiaji umeme.
Pamoja na maamuzi hayo, Bodi ya
Wakurugenzi wa EWURA, pia iliagiza
TANESCO kutekeleza yafuatayo:
kuzalisha umeme kwa
kutumia mitambo yenye
gharama nafuu ("least cost
merit order") na kuwasilisha
ripoti kwa Mamlaka katika
kila mwezi ikionyesha
uzalishaji halisi na mpango
wa uzalishaji kama
ilivyoidhinishwa na EWURA;
kuhakikisha kuwa zabuni za
miradi ya uzalishaji umeme
zinatolewa kulingana na
mahitaji kama
ilivyoidhinishwa kwenye
Mpango wa Umeme wa Taifa
(Power System Master Plan).
Miradi yote mipya lazima
ipatikane kwa njia ya
ushindani kwa kufuata
Sheria ya Umeme, "Public
Private Partnership Act",
Sheria ya Manunuzi ya
Umma na Kanuni husika;
kuwasilisha ripoti kila baada
ya miezi mitatu kuhusu
viashiria vya takwimu za
ubora na uhakika wa umeme
(supply and reliability) katika
misongo ya 11kV, 33 kV, 66 kV,
132 kV, na 220 kV kwa kila
mkoa kwa ajili ya uhakiki.
Takwimu husika zinatakiwa
kuonyesha jumla ya masaa
mteja aliyokosa umeme kwa
kila njia ya umeme ("feeder"),
kukosekana kwa umeme
kulikopangwa (planned
outages), na ambao
haukupangwa (unplanned
outages), idadi ya matukio ya
kukosa umeme katika kila
"feeder", idadi ya wateja
wanaohudumiwa na kila
"feeder", idadi ya wateja
walioathirika na katizo la
umeme katika kila "feeder"
na kiasi cha umeme
kilichokosekana kutokana na
katizo hilo (total unserved
energy in kWh);
kuwasilisha kwa Mamlaka,
katika kipindi cha miezi
mitatu baada kuanza kwa
Agizo hilo la Mamlaka,
mpango wa utekelezaji wa
"Demand Side Management
Programme" ili uidhinishwe;
kupunguza kiwango cha
upotevu wa umeme (technical
and non-technical losses)
katika mtandao wa
usambazaji kutoka asilimia
19 ya mwaka 2012 hadi
asilimia 15.1 ifikapo mwisho
wa mwaka 2015;
kubuni mikakati ya
kupambana wizi wa umeme
utokanao na uunganishaji
umeme usio halali, na
kuondoa ucheleweshaji usio
wa lazima katika
kutunganisha wateja wapya;
kuhamisha wateja walio
katika kundi la D1 kwenda T1
endapo matumizi yao ya
mwezi yatazidi uniti 75 kwa
miezi mitatu mfululizo;
kuwasilisha kwa Mamlaka,
kabla au tarehe 31 Machi,
2014, Mpango wa kuwawekea
wateja wake mita za LUKU na
AMR ili kupunguza wateja
wanaotumia mita za zamani
(conventional meters);
kuwasilisha kwa Mamlaka,
kila baada ya miezi mitatu,
taarifa/ripoti ya ukusanyaji
wa madeni kutoka kwa
wateja wake ili kuongeza
mapato ya Shirika;
kutoa elimu kwa wateja wake
kuhusu haki na wajibu wa
wateja kwa mujibu wa
Mkataba wa Huduma kwa
Wateja na kushughulikia
kero za wateja kama
inavyoelekezwa katika
Mkataba husika na Kanuni za
Umeme;
kuwasilisha kwa Mamlaka,
maombi ya marekebisho ya
bei yatokanayo na
mabadiliko ya bei za mafuta,
mfumuko wa bei na
ubadilikaji wa thamani ya
fedha; Ukokotoaji wa
marekebisho hayo utakuwa
kama ulivyoainishwa katika
Kanuni za Kupanga Bei za
Umeme za mwaka 2013
(Electricity (Tariff Setting)
Rules, 2013);
kuendelea kutoa taarifa kwa
Mamlaka kuhusu hali ya
kifedha na kiundeshaji.
Taarifa hizi zitatumiwa na
Mamlaka katika kutathmini
utendaji wa TANESCO
ikilinganishwa na mashirika
mengine ya umeme katika
nchi jirani ili kuboresha
utendaji wake. Tathmini hii
pia itatumiwa na Mamlaka
katika kubaini uhalali wa
maombi ya baadae ya
kurekebisha bei;
kuwasilisha kwa Mamlaka,
kabla au tarehe 31 Machi
2014, mpango wa utekelezaji
wa kila sharti katika Agizo la
EWURA.
Bei mpya za umeme zitaanza
kutumika tarehe 1 Januari 2014. Ni
matarajio ya EWURA kwamba
TANESCO watatumia fursa hii kutoa
huduma bora zaidi za umeme na
kuhakikisha kuwa wanashughulikia
malalamiko ya wateja kila
yanapojitokeza ili kurejesha imani
kwa Shirika la Umeme la TANESCO.
Post a Comment