Wapenzi wengi ambao wamefikia hatua ya kuachana wameshindwa katika vipimo vya kitalaamu kuthibitisha ubaya waliokoseana, ambao unaweza kubeba uamuzi huo mzito wa kuvunja ahadi zao za kimapenzi na hata ndoa.

Kwa mujibu wa watalaam wa masuala ya ndoa na mapenzi inaelezwa kwamba wapenzi wanaoachana huwa hawana sababu za msingi, hii inatokana na ukweli kwamba wanaoachana hawafahamu kiini kilichowatenganisha katika makubaliano muhimu na ya kwanza kabisa ulimwengu ya watu kufikia hatua ya kupeana utu wao.

Inasemwa hivyo kwa sababu ukilinganisha matatizo yanayotenganisha watu hayabebi hoja zinazokubalika na wapenzi wote. Kwa mfano kama wapenzi watasema wameachana kwa sababu wamefunaniana na wakadhani hiyo ni sababu wanakuwa wanaudanganya zaidi umma kwa maana kuna wanaofumaniana, wanaodhalilishana, wanaotukanana, wasioheshimiana kabisa, lakini bado wanadumu katika ndoa zao bila kuachana.

Kwa ulinganifu huo, wachunguzi wa mambo ya ndoa wanasema, kuachana si zao linaloota na kukua kwa siku moja, bali ni migogoro isiyoshughulikiwa kwa muda mrefu ambayo huwaachanisha wanandoa taratibu bila wao kujua.

Kwa maana hiyo wanaoachana au watakaoachana wanatakiwa kufahamu kuwa safari yao ya talaka haianzi na kumalizika kwa siku moja, isipokuwa hufikia katika hitimisho baada ya kuwepo katika mwendo kwa muda mrefu, ambapo dalili zake huwa hizi zifuatazo:

1 : Ikiwa mmeoana na baadaye mkaanza kuonana ni watu msiohitajiana sana katika maisha. (mapenzi kuchuja). Kila mtu anafahamu kuwa wakati wa uchumba mapenzi huwa moto moto lakini baada ya kuoana hujitokeza hali ya kuanza kuzoea. Hii inatokana na ukaribu ambao mwanzo haukuwepo au kusitishwa kwa machimbezo yaliyokuwa yakiboresha uhusiano. Kwa mfano wapenzi wengi wanapokuwa kwenye uchumba hufanyiana mambo mengi yakiwemo ya kutumiana zawadi na kadi au kutoka pamoja kwa matembezi, lakini wakioana hujikuta hawafanyiani hayo, jambo ambalo huathiri mapenzi yao.

Uchuchuzi unaonyesha kuwa wapenzi walio kwenye uchumba wanapokuwa pamoja hutumia muda mwingi sana kuomngea kwa simu, kutumiana meseji, kuzungumza tofauti na mume na mke. Ukitaka kuthibitisha keti barabarani ukiona mwanaume na mwanamke wamo ndani ya gari hawaishi kucheka na kuzungumza wafuatilie utakuta mwisho wa safari yao wanaagana kila mmoja anakwenda kwake (ina maana si mume na mke hao). Ni nadra sana kuwakuta wanaume wakiwa pamoja na familia zao wakifurahi, jambo ambalo hupunguza upendo na kuleta mazoea na hisia za kutohitajiana sana. Hili halifai likiwepo ni ishara kuwa mapenzi yanakaribia kunyauka.


2 : Mkiwa hamsameheani na kusahau mnapokoseana. Si watu wengi ambao wako tayari kusamehe na kusahau makosa. Wapenzi wa dunia ya leo wakisema nimekusamehe haina maana wamefuta kosa bali hiliweka kando na kulikumbushia wakati mwingine. ‘Hili ni kosa la tatu tarehe fulani ulinifanyia hivi, wiki iliyopita na jana kulinijibu hivi hivi sasa leo siwezi kukuvumilia”
Kauli kama hizi hutoka kwenye vivywa wa watu ambao hawako tayari kusamehe, kosa la mwaka juzi litakumbushwa tena na tena na kuzidi kuchochea ugomvi hata uliokuwa mdogo na kuoneka mkubwa kwa sababu tu umehusishwa na makosa yaliyopita. Inashauriwa kuwa uhai wa mapenzi lazima uambatana na kusameheana kama wanadamu na kusahau makosa. Hili lisipofanyika ni rahisi kuua penzi na kuwafanya watu kuachana. Ni vema kila mmoja wetu akajichunguza tabia yake na kuacha kukumbusha makosa yaliyopita.


3 : Msipokubali kuwekeana mipaka ya kiutawala. Kuna suala linatambulishwa sana siku hizi na wanaharakati, linaitwa usawa wa kijinsia, jambo hili limekuwa likichangia sana migogoro ya ndoa hasa baada ya kutumiwa vibaya na wahusika. Hakuna ubishi mila za kiafrika zinaongozwa na mfumo dume, kuubadili mfumo huu kwa haraka kumekuwa kukiharibu uhusiano mwingi wa kimapenzi kutokana na ukweli kwamba ni wanaume wachache sana ambo wako tayari kuishi na wanawake wanaovutana nao kimamlaka.

Hivyo ili kunusuru hili lisiwe kikwazo katika mapenzi tunashauri kila mwanandoa kuheshimu mipaka yake na kujali zaidi utu na si usawa kama inavyotambulishwa (haya ni mawazo yangu). Watu wanaojali utu katika familia watakuwa tayari kuwapa heshima wanaoishi nao kwa kusikiliza mawazo yao na kutokutumia nguvu kuwakandamiza wengine. Ni vema mwanamke akachungua nafasi yake kwa mumewe na mume naye akamuheshimu mke kwa utu wake.


4 : Msipozungumzia vikwazo vya maisha.

Matarajio ya watu wengi wanapokuingia katika uhusiano wa kimapenzi huwa ni kupata faraja, ni wachache kati yao hufikiria kukutana na vikwazo vya kimaisha. Tafiti zinaonyesha kuwa wakati mtu anapotafuta mpenzi huamini toka moyoni kuwa akiwa na waridi wake matatizo ya upweke, kukosa msaada wa hili na lile yatakwisha lakini baadaye anakuja kubaini kuwa aliyokusudia kuyapata hayapati tena na hivyo kujuta kwa kauli kama hizi. “Kama ningejua kama mwanaume mwenyewe yuko hivi nisingekubali kuolewa.”

Kauli kama hizi mara nyingi hutokea kwa watu ambao hawazungumzii matatizo na vikwazo wanavyokutana navyo katika mapenzi na kuviondoa. Kama mpenzi wako ana matatizo unasubiri nini kuyatafutia ufumbuzi au kama maisha hayaendi sawa ukimya wa nini kwa mwenza wako, kaeni chini muambizane kuwa mnaupungufu wa fedha na dhiki kadhaa wa kadhaa, ili kama kutatokea kukosa mahitaji muhimu liwe ni jambo linaloeleweka na wote kuwa linatokana na kipato kushuka. Uchunguzi unaonyesha kuwa wanaume wengi wanapokukwama kiuchumi hupunguza matumizi kimya kimya jambo ambalo huwafanya wanawake wengi kubaki wakitumikia zana potofu kuwa huenda wananyimwa baada ya kuwepo kwa nyumba ndogo.

5 : Msipokuwa na mipango ya pamoja na uwazi wa matumizi ya pesa.

Nina ushahidi wa kutosha juu ya kuwepo kwa wapenzi hasa wenye kipato kutokuwa wawazi katika mipango yao ya kimaisha na matumizi yao pesa. Natambua baada ya kufanya uchunguzi wangu kuwa pesa za baadhi ya wanawake huwa hazina matumizi ya wazi, badala yake wanaume hubanwa kwa kisingizio kuwa wao ndiyo wana wajibu wa kutunza familia.
Hali hii imekuwa ikileta migogoro mingi sana kwenye familia na kushusha upendo kwa vile upande unaohudumia familia hapa haijalishi mume au mke huwa unajikuta ukikereka kwa kukosa msaada wa upande wa pili na hivyo kuondoa mapenzi ya kweli. Kama hilo halitoshi vijana wengi wa kiume siku hizi wamejikuta wakiahirisha mapenzi yao kwa wasichana baada ya kukosa ushirikiano wa kimapato na matumizi yake.

“Ninashida ya kuonana na wewe mpenzi wangu, vipi nikufuate kazini?” Jibu linakuwa “Hapana niko bize sana leo.” Inawezekana kabisa mtu akawa hayuko bize lakini kwa sababu anaogopa kukamuliwa kipato na yeye mambo yake hayako sawa anaamua kukacha ahadi. Lakini ukiwepo ushirikiano wa kimatumizi husaidia kudumisha mapenzi.
Inashauriwa kwamba kama wapenzi wote wana kazi na wanapokea mishahara ni vema vipato vyao vyote vikatumika katika kutunza na kuendeleza familia. Tabia ya mwanamke kumtegemea mwanamume kimatumizi huku yeye akitumia pesa zake kwa manunuzi ya vipodozi na nguo au kufanyia mambo yake kwa siri haijengi badala yake inanyausha mapenzi kama siyo kuyaua kabisa.

6 : Mkiacha kujaliana na kupeana haki katika tendo la ndoa.

Tendo la ndoa ni muhimu kwa wanandoa kwa vile linahusika na hizia za mwili. Matatizo mengi ya usaliti kwa mujibu wa uchunguzi, yanatokana na wapenzi kutotoshelezana wakati wa tendo la ndoa. Kwa kutokutambua madhara au kwa uzembe, wapenzi wengi wamekuwa wakiacha kutimiziana tendo hilo bila kuwepo kwa sababu za msingi. “Mimi nimechoka siwezi kufanya mapenzi.”
Inawezekana kweli mtu akawa kachoka sawa na kauli hiyo lakini sababu hiyo haiwezi kumfanya mwenza akazimaliza hisia zake, isipokuwa kwa kutafuta njia mbadala zikiwepo za usaliti. Sambamba na hilo wapenzi wengi wamenyausha mapenzi yao kwa kutokuwa wabunifu katika uwanja wa sita kwa sita kwa kutokujituma, kutobuni staili mpya, kutochombeza na kutohamasisha kwa cho chote na kibaya zaidi kutokuwepo kwa usafi wa mwili yao.

Katika kipindi cha maisha yangu ya ushauri wa masuala ya saikolojia, maisha na mapenzi nimekuwa nikikutana na wanaume wengi wanaolalamika kuwa wana upungufu wa nguvu kiume. Lakini wengi kati ya hao ambao mamia yao nimeshawasaidia walijikuta wakipungukiwa nguvu zao kwa sababu za kisaikolojia zilizochochewa pia na udhaifu wa wenza wao. Kama utakuwa na mtu kwa mfano, ambaye mtakutana naye chumba kile kile, eneo lile lile, staili zile zile, kwa miaka mitano mfululizo bila shaka hali ya kukinaishwa itakuwepo na hivyo mapenzi kunyauka. Katika hili ni vema kujifunza zaidi namna ya kutoshelezana katika tendo la ndoa.

7 : Mkibeba fikra binafsi kwa kila mtu kutaka mafanikio yake.

Maisha ya wapenzi wengi yamekuwa yakipoteza maana kiasi cha kufikia kuchuja kutokana na wapenzi wenyewe kuwa na mawazo ya ubinafsi. Utakuta watu wameoana lakini kila mmoja anakabili changamoto za maisha peke yake, hali ambayo humfanya atumie nguvu kubwa kutafuta ushindi wa matatizo yake.

Mantiki ya maisha ya ndoa ni kusaidiana. ‘Mungu alimwambia Adamu kuwa atampatia msaidia wa kufanana naye ambaye ni mwanamke aliyeitwa Hawa.’ Upo pia msemo usemao ‘Kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi’ Ni wajibu wa wanandoa kuhakikisha kuwa maisha yao yanakuwa ya nyuzi mbili ili yasikatike upesi. Lakini ikiwa kila mtu anajenga nyumba yake, anafanya biashara zake, ana mipango yake binafsi ujue mwisho mbaya wa mapenzi umesogea.

8 : Mkiwa watu wa kutoa siri zenu nje.

Upo udanyanyifu mwingi wa kimawazo miongozni mwa wapenzi wengi kiasi cha kudhani kuwa kumwambia rafiki au ‘shoga’ masuala ya ndani ya ndoa ni kutafuta suluhu ya matatizo. Hii si sahihi kwa vile upo ushahidi mkubwa juu ya wapenzi wengi ambao walijikuta katika wakati mgumu baada ya kutoa siri zao nje. Ifahamike kuwa ndoa imara ni ile inayoheshimika katika jamii, na heshima hiyo haiwezi kuwepo kama wanandoa hawatakuwa makini katika kutunza siri za mapenzi yao.

Haipendezi kwa mwanamke/ mwanaume kwenda kijiweni na kuanza kuanika mambo ya ndani kwa mfano. ‘Yaani leo mume wangu hakuacha kitu chochote ndani sijui itakuwaje. ‘Sema wanawake wote lakini si mke wangu, ana kasoro nyingi sana.’
Kauli kama hizi na nyingine ambazo zinatoa nje udhaifu wa maisha yenu hazifai, kwani katika kila ndoa kuna udhaifu mwingi ukiwepo ukimya ina maana wahusika wanaweka udhaifu wao kifuani kwa maslahi ya maisha yao. Na wewe uwe hivyo kwa kutunza siri za mumeo.mkeo.

9 : Msipokuwa wawazi katika kuzungumzia upungufu wa kibinadamu mlionao na kusaidiana.

Wapenzi wasomaji wangu, hakuna mwanadamu aliyekamili kwa asilimia mia moja. Ukimuona hodari wa hili ni dhaifu wa lile, kinachotakiwa ni kusaidiana katika kufikia ukamilifu. Faraja inayopatikana katika upungufu wa mwanadamu hasa usiokuwa wa kimaumbile ni kuwepo kwa utatuzi wake. Kuna wapenzi wengi wamefikia kuachana kwa kasoro ndogo ndogo kama za kutojua mapenzi, au hata uchafu wa mwili ambao kama wangekaa na kujadiliana pamoja wangepata ufumbuzi wa tatizo.

Inashauriwa kuwa kunapokuwepo upungufu wowote wa kati ya mwanaume na mwanamke ni wajibu wa wapenzi wenyewe kukaa chini na kuelezana wazi na kushirikiana katika kupata ufumbuzi. Unashindwa nini kuwambia mpenzi wako kuwa hakutoshelezi katika tendo la ndoa, ana harufu mbaya mwilini, mchafu, hajui mapenzi na mambo kama hayo! Kikubwa katika hili ni kujua namna ya kuwasil;isha ujumbe, maana kuna wengine hawana lugha nzuri za mawasiliano “Yaani mke wangu unanuka sana mimi nakerwa sana” Ukisema hivi utamfanya mwenzako aone kama unamnyanyapaa. Tumia lugha nyepesi itakayosaidia kumaliza tatizo msikae kimya bila kuzungumzia upungufu wenu mtajikuta mnaachana.

10 : Mkiendekeza nguvu katika kutwaa madaraka ndani ya familia.

Kuna baadhi ya familia kila mmoja ni mtemi hakuna diplomasia katika kutatua migogoro. Utakuta mwanamke ni mbogo na mwanaume naye ni simba, basi shughuli inakuwa nzito. Ndoa inakuwa uwanja wa ndodi kila siku kutoana manundo. Hakuna mapenzi ya namna hiyo! Kanuni za mapenzi bora zinakataza wapenzi kutumia nguvu kutwaa madaraka au haki ndani ya familia. Inawezekana kabisa wewe kama mke/ mume ukwa na haki katika jambo fulani lakini haki hiyo haikupi fursa ya kutumia nguvu nguvu kuipata.

Kinachotakiwa katika mapenzi ni kuheshimiana, kwani katika hali ya kawaida utumiaji wa nguvu katika kudai haki ndani ya familia ni moja kati ya mambo yaliyoshindwa katika historia kuleta maelewano. Kama unadhani naongopa keti chini ujitathmini tangu umeanza kumchunga mumeo/mkeo na kumbana kwa ngumi umepata mafanikio gani, ameacha tabia yake au ndo anazidi? Umwamba haufai kutumika katika maisha ya ndoa kwa mtu yoyote awe mwanaume au mwanamke.

11 : Mkiwa watu msioheshimiana mbele za watu na kupenda zaidi kusema kuliko kusikiliza.

Nimeshuhudia wapenzi wengi ambao hawajui umuhimu wa kuheshimiana mbele za watu. Utakuta mwanamke/mwanaume akimwaibisha mwenzake mbele za watu kwa kumfokea, kumwita jina baya, kumtusi, kumtoa kasoro na hata kumdhalilisha. Kitendo hiki ni kibaya na maumivu yake hudumu kwa muda mrefu akilini mwa mtendewa.
Inashauriwa kwamba wapenzi wanapokuwa mbele za watu wachunge ndimi zao na wawe watu wanaopenda zaidi kusikiliza kuliko kunena. Inaelezwa, penye wingi wa maneno yapakosi kuwa na uovu. Kuna wanawake wakianza kuwatusi waume zao mpaka nyumba ya 50 wanasikia au wakati mwingine hutoka nje na kumwaga mitusi kana kwamba wameambiwa watapewa tuzo. Hiyo si heshima na hajawahi mtu kuheshimika kwenye jamii kwa uhodari wa kutukana watu.


12 : Msipokuwa tayari kukubali kosa na kujirekebisha.

Dalili nyingine ya mapenzi kunyauka ni kwa wapenzi wenyewe kuwa na tabia ya kutokukubali makosa na kujirekebisha. Utakuta mwanaume/,mwanamke ameshaambiwa mara nyingi na mwenza wake juu ya tabia zake na pengine hata marafiki zake wamemtahadharisha lakini habadiliki, kila siku anarudia makosa yale yale ambayo yanamuumiza mpenzi wake. Huu ni mwenendo mbaya, ubinadamu unamtaka kila mtu kuwa tayari kukiri kosa na kujirekebisa

13 : Msipokuwa watu wa kuitafuta furaha pale inapokosekana.

Wakati mwingine harakati za maisha huleta huzuni, kwa mfano, kama wanandoa watafiwa, kuuguza, kufukuzwa kazi, kupoteza mali kwa kuibiwa na matukio kama hayo huondoa furaha. Hapa inashauriliwa kwamba endapo furaha itaondoka kwa sababu yoyote wanandoa wanajukumu la kuitafuta. Hapa namaanisha kutiana moyo na kuwezeshana kusonga mbele wakiamini kuwa hakuna marefu yasiyokuwa na ncha. Kuacha huzuni itawale nyumba yenu kwa muda mrefu hupunguza mapenzi.

14 : Msipozingatia kuombana msamaha bila kujali nani mwenye kosa.

Kuombana msamaha ni jambo la lazima kabisa katika ndoa, na busara inamtaka mwenza kuwa tayari kuomba masamaha hata kama anaona kabisa hakuna kosa la msingi alilolifanya mbele ya mwenzake. Kung’ang’ania kutaka haki kipindi cha kuzozana ni njia ya kuelekea kukosana zaidi na hatimaye kuachana. “Nakuomba unisamehe mke/mume wangu, najua nimekuudhi.” Baada ya kutoa kauli hiyo na mzozo kupoa mhusika anaweza kufafanua kilichotokea na hapo anaweza kueleweka zaidi kuliko kipindi ambacho mpenzi wake anakuwa na hasira.

15: Msipokuwa tayari kukumbushana wajibu na mwenendo wenu

“Atajijua mwenyewe siku yakimkuta ya kumkuta huko ndo atafahamu” “Mimi nimechoka nimebaki namwangalia tu.” Kubaki unamwangalia mpenzi wako anaharibikiwa si uamuzi wa busara kwani mwisho wa siku kama ni aibu itakufikia na wewe pia. Ukimuona mwenzako anakwenda nje ya mstari wa jamii mrejeshe na kuzidi kumkumbusha kila siku wajibu wake kama baba au mama wa familia, hii inasaidia kumuweka sawa mahali anapokosea.


Mpaka hapa tutakuwa tumefikia tamati ya somo letu, naamini watu wengi wamejifunza vya kutosha. Shukrani za pekee ziwaendee watu wote waliokuwa pamoja nami tangu mwanzo wa somo hili

Post a Comment

POPULAR POST

 
Top