Aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, amesema atafanya kazi kukijenga chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Tanzania) kwa kukipaisha kama alivyofanya kazi akiwa ndani ya Chadema.
Amesema akiwa kiongozi Chadema kwa miaka zaidi ya 20 alifanya kazi ya kukijenga chama na kuhakikisha kinatoka kuwa na wabunge wanne na sasa kimepanda na kuwa na wabunge 48.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Zitto alizitaja sababu tano zilizomfanya ajiunge na ACT-Tanzania ikiwamo kuvutiwa na msingi mama wa chama hicho wa kuweka mbele masilahi ya Taifa.
“Nataka kuwakumbusha wakati napewa uongozi huko nyuma nilishiriki kujenga chama ambacho kina wabunge wanne tu na kuna wakati tukienda kwenye mikutano tunakuta watu 20, lakini tulifikisha hadi wabunge 48.
“Na mimi ni mchapa kazi na sasa nimeamua kuingia kufyeka pori na nitalifyeka pori na tukikutana Novemba tutakuwa na majibu ya maneno yangu…,” alisema Zitto.
Akizitaja sababu tano za kujiunga na ACT-Tanzania alisema katu hatorudi nyumba kupambana kwa ajili ya rasilimali za Taifa na watu wake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nchi inakuwa katika misingi ya uadilifu na uwajibikaji kwa umma.
“Nimekuwa nikipigania uzalendo kwa nchi yangu tangu nilipoanza siasa na nimekuwa nikiweka mbele masilahi ya Taifa dhidi ya kitu kingine chochote,” alisema Zitto.
Sababu ya pili unatokana na chama hicho kuwa pekee kinachokubaliana na itikadi ya ujamaa na kinaamini katika falsafa ya Nyerere iliyo na lengo la kurudisha nchi katika misingi iliyoasisi taifa.
Kutokana na hali hiyo, Zitto alisema anaamini kuwa ACT itasimama katika misingi ya uadilifu na kimeweka miiko na maadili ya viongozi katika kuhakikisha viongozi wa chama hicho wanatakiwa kukubaliana nayo kwa kusaini.
“Katika miaka yangu ya ubunge nimekuwa nikipigania uwajibikaji na uwazi jambo ambalo ninaliamini kwa moyo wangu kwenye utumishi wangu kwa umma.
“Nimefurahi kwamba kati ya misingi 10 ya ACT, uwajibikaji na uwazi ni misingi ambayo naamini inatokana na utumishi wa umma na suala la uwazi limekuwa sehemu ya jina la chama hicho hivyo kwangu ACT ni nyumbani katika siasa na katika utumishi wa umma,” alisema Zitto.
Zitto alisema amejiunga ACT kwa sababu amekubaliana na imani yao ya kujitegemea, bidii, umakini na weledi katika kazi kuwa ndiyo msingi wa maendeleo.
Sababu nyingine aliyotoa ni kukubaliana na imani ya ACT kwamba umoja ni ngao muhimu katika ujenzi wa taifa na Afrika kwa ujumla.
Alisema kwa sababu hiyo ameona upo umuhimu wa kurudisha nchi katika misingi iliyoliasisi taifa.
“Lazima tuirudishe nchi katika heshima ya uongozi wa Bara la Afrika hivyo naahidi kufanya kazi na makundi yote, wanaoamini katika siasa safi na siasa za hoja, tunataka kufungua kurasa mpya wa siasa nchini."
Usaliti
Akizungumzia kuhusu wanaomtuhumu kufanya usaliti, Zitto alijibu kwa kutumia nukuu za Rais wa kwanza wa Ghana, Kwame Nkurumah akisema haangalii nyuma tena bali anaangalia mbele.
“Naombeni mjaribu kufumba macho yenu mjiulize ni mbunge gani katika Bunge hili ambaye ametoa hoja ambazo zilikitikisa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mara mbili nimetoa hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, taarifa yangu wakati ule nikiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), mara mbili nimeng’oa mawaziri wa CCM, mwaka 2011 mawaziri wanane.
“Juzi juzi katika suala la Escrow nimewang’oa mawaziri watatu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hivyo, swali kama hilo la usaliti lilitakiwa kupewa wale ambao wako bungeni na hawafanyi kazi ya kuiwajibisha serikali si kwa mtu ambaye maisha yake yote ya ubunge amefanya kazi ya kuiwajibisha serikali,” alisema.
Mafao Yake
Alipotakiwa kuelezea kuhusu masilahi yake ya ubunge, Zitto alisema kwake masuala ya fedha halina nafasi kwa sababu yupo kwa sababu ya kusimamia masilahi ya Watanzania.
“Tangu mwaka 2011 nimekuwa mbunge pekee ambaye nimekuwa sipokei posho ya Bunge hadi naondoka bungeni kwa hivyo basi uamuzi wangu wa siasa hauangalii fedha bali hoja kwangu ni kuona tunapoelekea,” alisema.
Vigogo wajiunga
Wakati wa mkutano huo Zitto jana, chama hicho cha ACT-Tanzania, kilivuna wanachama wapya zaidi ya 10 wakiwamo waliokuwa viongozi wa Chadema katika ngazi ya mikoa na wilaya.
Waliojiunga na chama hicho ni pamoja na aliyekuwa mgombea ubunge wa kura za maoni CCM katika jimbo la Kasulu Mjini, Askofu Dk. Gerald Mpango, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu Kanda ya Magharibi Chadema, Jaji Mstaafu Mussa Kwikima.
Mwingine ni Kansa Mbarouk aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, Jorum Mbogo aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kaliua, mgombea ubunge wa jimbo la Temeke mwaka 2010 Chadema, Dickson Ng’ili.
Wengine ni Meck Mzirai aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora na Mjumbe wa Kamati Kuu, Charles Lubala Mwenyekiti wa jimbo la Kahama na mgombea ubunge 2010 Chadema na Diwani wa Mabogini Halmashauri ya Moshi, Albert Msando (Chadema).
Pia wamo Dk. Ben Kapwani aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa, John Malaki Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Katavi, Mwasimtwa Mwagongo, Kaimu Mwenyekiti wa TLP Wilaya ya Mbarali na Katibu wa TLP Wilaya ya Mbarali, Selemani Nyumile.
Wabunge 10 Kujiunga na ACT
Wabunge 10 Kujiunga na ACT
Akizungumza na Mwandishi wetu jana jijini Dar es Salaam, baada ya kuzungumza na waandishi wa habari, Zitto alisema nyuma yake wapo wabunge zaidi ya 10, watakaojiunga na ACT muda sio mrefu.
“Siko mwenyewe wapo wenye mapenzi mema na tunataka kufungua ukurasa mpya kwa nchi yetu wa siasa za kujenga nchi, wabunge mahiri wa CCM na Chadema zaidi ya 10, watajiunga nami, ila sitakutajia majina kwa sasa kwa sababu ya sheria za vyama vyao, acha wamalizie vipindi vyao vya ubunge,” alisema Zitto
Post a Comment