Dr. Clifford B. Majani
Mkomamanga (Punica granatum)ni mmea ambao asili yake ni katika nchi za Mashariki ya Kati (Middle East) na umetajwa sana katika vitabu vya kale vya historia ya eneo hilo. Kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyoandikwa na Taasisi ya Utafiti wa Kiswahili (Institute of Kiswahili Research) ya
Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam-Tanzania, mkomamanga ni mti unaozaa
matunda ambayo maganda yake huchemshwa na kufanywa dawa ya kufunga
kuhara (TUKI, 1981).
Hii inaonyesha kuwa wenyeji wa Upwa wa Afrika Mashariki wamekuwa na
uzoefu wa kutosha kuhusiana na uwezo wa tiba wa mmea wa mkomamanga kwa
muda mrefu hasa ikizingatiwa kuwa wamekuwa na mfungamano wa kihistoria
na wageni toka Mashariki ya Kati kwa kipindi kirefu.
Mkomamanga una dawa mbalimbali kama vile Tannis (punicalin na
punicalagin), Flavonoids, Alkaloids, Steroids, Triterpenes na
Polyphenols. Dawa hizi hupatikana katika magome, majani, mbegu, maganda
ya matunda, juisi ya matunda na katika maua ya mkomamanga. Tunda la
komamanga pia lina vitamini C na E kwa wingi pamoaja na madini ya
potassium na copper.
Faida za kitabibu za mmea-dawa huu
Katika majaribio ya kisayansi imethibitika kuwa juisi ya komamanga na
fukuto ya mmea huu husaidia kudhibiti kasi ya kuzaliana kwa virusi vya
UKIMWI namba 1 [HIV-1]. Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na
Neurath A. R pamoja na wenzake na kupewa kichwa kisemacho “Punica
granatum juice provides an HIV-1 inhibitor and candidate tropical
microbicide”. Utafiti huu ulichapishwa katika jarida la kisayansi la BMC
infectious diseases (4) 41-45(2004). Matokeo yanayofanana na hayo pia
yalithibitika katika utafiti mwingine uliofanywa na Kun Silprasit na
wenzake mnamo mwaka wa 2011 na kupewa jina la “Anti-HIV-1 Reverse
transcriptase activities of hexane extracts from Asian Medicinal
Plants”. Utafiti huo ulichapishwa katika jarida la kisayansi la “Journal
of Medical Plant Research Vol. 5 (17), pp. 4194-4201, 9 Sept 2011”.
Dawa zinazopatikana katika maganda na
majani ya mkomamanga husaidia katika matibabu ya hali ya tumbo kujaa
gesi na kudhibiti tindikali (acid) tumboni. Mkomamanga pia husaidia katika matibabu ya kuhara damu na kutibu uambukizo katika kibofu cha mkojo (Cycititis).
Lojo ya mbegu za matunda ya komamanga
ikichanganywa na maziwa, husaidia katika tiba ya kuondosha mawe katika
figo. Fukuto ya Mkomamaga husaidia katika tiba ya minyoo aina ya tegu (Tapeworms) lakini pia husaidia katika matibabu ya uvimbe wa wengu (Spleen). Dawa-lishe hii pia husaidia kwa kiwango kikubwa katika uponaji wa vidonda vya tumbo.
Katika jaribio moja lililofanywa kwa
wanyama, dawa hii ilionyesha uwezo mkubwa sana (97.4%) wa kuponya
vidonda vya tumbo. Kazi hii hutokana na uwezo wa dawa hii wa kudhibiti
bakteria aina ya Helicobacter pylori
ambao kwa kiasi kikubwa huchangia kutokea kwa vidonda vya tumbo (70
-80% ya vidonda vya mfuko wa chakula na 90% ya vidonda katika utumbo).
Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Hu W. na wenzake mnamo mwaka
2006 na kupewa kichwa kisemacho “Study of in-vitro inhibition effect of
Pomegranate rind on H.pylori”. Utafiti huu ulichapishwa katika jarida la
Academic Journal of Kunming Medical College 27, 25-27.
Utafiti mwingine uliofanywa na H.R. Rahimi na wenzake mnamo mwaka 2011
ujulikanao kwa jina la “Punica granatum is more effective to prevent
Gastric Disorders Induced by Helicobacter pylori or any other stimulator
in humans” uliochapishwa katika jarida la kitabibu la Asian J. of Plant
Sciences 10 (7): 380-382, 2011; pia ulithibitisha uwezo wa mkomamanga
katika tiba ya vidonda vya tumbo. Lakini pia uwezo wa dawa hii wa
kupunguza uzalishaji wa tindikali tumboni, huchangia katika uponaji wa
haraka wa vidonda vya tumbo.
Katika mfumo wa damu, komamanda hutoa
msaada mkubwa wa kuzuia na kutibu magonjwa yanayoshambulia mfumo huo
nyeti. Komamanga ni dawa nzuri ya kuzuia na kutibu shinikizo la damu,
magonjwa ya nyama za moyo, kiharusi (Cerebrovascular Accident)
na magonjwa ya mishipa ya damu. Komamanga lina madini aina ya potassium
na copper kwa wingi, pamoja na faida zingine mwilini, madini haya
husaidia kusharabiwa (kufyonzwa)
kwa madini ya chuma kutoka katika utumbo kwenda mwilini kwa urahisi na
hii husaidia katika matibabu na kinga ya tatizo la upungufu wa damu
mwilini.
Komamanga pia ni mahili katika tiba na kuzuia magonjwa ya kusendeka (magonjwa ya muda mrefu) kama vile saratani ya tezi ya prosteti ya wanaume, saratani mbalimbali, kisukari, baridi yabisi na uvimbe wa maungio ya vidole (gout). Komamanga husaidia mwili kuondosha sumu na uchafu utokanao na kemikali na mabaki ya vyakula mwilini kama vile asidi ya uriki (uric acid). Sumu hizi ni chanzo kikuu cha magonjwa mengi ya kusendeka.
Komamanga pia husaidia katika jitihada za kukabiliana na tatizo la unene wa kupindukia (Obesity). Husaidia katika matibabu ya tatizo la ini pale linapolemewa (Liver congestion).
Dawa ndani ya komamanga licha ya kuwa na uwezo wa kudhibiti aina kadha
wa kadha za bakteria wanaosababisha magonjwa mwilini, pia zina uwezo wa
kukabiliana na virusi wa aina mbalimbali wanaosababisha magonjwa kwa
binadamu.
Kwa mujibu wa wasomi na wanazuoni wenye shahada za uzamivu, Dk. Navindra Seeram na Dk. Risa Schulman, komamanga kwa hakika ni dawa asilia inayotamba katika tiba za kisasa (Modern Medicine) kwenye karne ya 21.
Kipimo
Dawa-lishe hii hutumiwa kwa kunywa fukuto inayotokana na sehemu za mmea
kiasi cha gram 3 hadi 9 kwa siku inatosha kwa ajili ya tiba ya magonjwa
mbalimbali. Kwa ajili ya minyoo ya tegu magome au mizizi ya mkomamanga
kiasi cha gram 50 huchemshwa katika lita 1 ya maji ili kupata fukuto.
Juisi ya matunda yake pia inaweza kutumiwa kiasi cha bilauli moja kila
siku ili kukinga magonjwa mbalimbali. Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali
dawa hii ni salama kama itatumiwa kulingana na kipimo sahihi. Tahadhari
ichukuliwe kuhusu matumizi ya dawa hii kwa wanawake wajawazito na kwa
watoto chini ya umri wa miaka 12 kwani hakuna taarifa za kutosha
kuhusiana na usalama katika makundi haya.
Madhara yanayoweza kutokea kwa kutumia dawa-lishe hii (Adverse reactions)
Matumizi ya kipimo kikubwa cha dawa hii ikiwa katika hali yake ya asili (zaidi ya gram 80)
kinaweza kusababisha kizunguzungu, maumivu makali ya kichwa, kushindwa
kufumbua macho, kutapika, kuzimia na wakati mwingine inaweza kusababisha
kifo. Dawa hii pia inaweza kusababisha mwili kunyong’onyea, kutokuona
vizuri, kushitukashituka kwa misuli na kutetemeka kwa mikono kama mlevi (tremors).
Onyo:
Ni vizuri kuepuka matumizi holera ya dawa hata kama ni dawa za asili. Si
kila dawa ya asili ni salama kama itatumiwa bila kufuata ushauri wa
mtaalamu aliyesoma na kuelewa vizuri sayansi ya tiba asilia na lishe.
Mimea ina kemikali za asili hivyo inapotumiwa ni lazima tahadhari
zichukuliwe kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.Kumbuka mimea ni dawa.
Post a Comment