Ni siku nyingine shughuli zinaendelea, kila mmoja anahangaika kutafuta riziki hata hivyo mamia ya wanaume kati ya wale wanaoonekana wakitembea barabarani na kuendelea na shughuli zao kama kawaida wana siri nzito inayowatafuna…ndani ya maisha yao.

Imezoeleka kuwa wanawake ndiyo viumbe pekee wanaopata manyanyaso toka kwa wenza wao, jambo ambalo lilisababisha vita kali kuanza…vita ya kumtoa mwanamke katika manyanyaso, ukatili, udhalilishaji na kadhia zote zinazotajwa kusababishwa na maumbile yake.

Hata hivyo, ukifuatilia kwa karibu, pengine kusikiliza visa vingi vinavyotokea katika mitaa ya hapa nchini, utagundua kuwa wanaume nao, wananyanyasika kwa kiasi kikubwa kama wanawake wanavyonyanyasika.

Kwa bahati mbaya, wengine wamekuwa wakificha manyanyaso hayo kwa sababu ya aibu au kwa sababu tu wao wanaamika kuwa ni jinsia shupavu, basi wanaona si vyema kuliweka wazi tatizo linalowaumiza na kuwafadhaisha.

Pengine wanaona ni fedheha, aibu au labda si jambo lililozoeleka katika jamii hasa za Kiafrika. Lakini huu ni wakati mwafaka wa kuuweka wazi ukweli kuhusu manyanyaso mnayoyapata.

Kwa mfano, nilipigiwa simu hivi karibuni na mwanamume wa miaka 42 ambaye jina lake nalihifadhi. Alisema kuwa mwaka 2010, aliugua ugonjwa wa kisukari ambao ulimsababisha kupoteza nguvu zake za kiume. Mke wake, hakuvumilia mabadiliko hayo, bali alianza kutoka nje ya ndoa.

“Mwanzoni alificha, lakini baadaye aliona ni haki yake kufanya hivyo na alianza kuwa jeuri, akinitukana na akirudi usiku au wakati mwingine ninasikia gari likimshusha nje,” anasema.

Anasema, alijaribu kumkanya kuhusu tabia hiyo, lakini alikuwa na kiburi kupita kiasi. Kadri siku zilivyoendelea alianza kumsimanga kutokana na hali aliyonayo. “Kibaya zaidi nilipokuwa nikimkanya, alitishia kuwa atawaambia ndugu na rafiki zangu kuwa mimi si mwanamume kamili,” Anasema mwanamume huyo kwa masikitiko.

Wapo wanaume wengi wanaopitia changamoto kama hizi au za aina nyingine, lakini wamezimeza na kuzifungia katika uvungu wa mioyo yao, wakiogopa fedheha.

Umefika wakati wa kusema ukweli kuwa wanaume nao wanapata manyanyaso, ili kama ni vita kwa ajili yao, ianze tena kwa makali kama ile inayofanyika kwa ajili ya wanawake.

Pia, wanaume walio wengi wananyanyasika zaidi pindi wanapoanguka kiuchumi, kwa mfano, mwanamume mwingine alizungumza na gazeti hili na kusema jinsi mke wake alivyomtupia virago nje ya nyumba mara baada ya kufukuzwa kazi katika benki moja hapa nchini.

“Wakati namuoa, nilikuwa ni meneja wa NMB. Tulipendana sana, lakini baada ya miaka mitatu ya ndoa, nilifukuzwa kazi kwa sababu ambazo sitaki kuzitaja. Alipoona nimekaa nyumbani mwaka mzima sina kazi, alianza vituko. Akaamua kunifukuza akidai mali zote nilizochuma ni zake,” anasema mwanamume huyo.

ata kutoka Ofisi ya Takwimu kutoka Uingereza, zinaonyesha kuwa, asilimia 40 ya wanaume duniani kote wanapata manyanyaso kutoka wake zao. Takwimu hizo za 2010 zinaonyesha idadi ya wanaume wanaonyanyaswa na wenza wao ilianza kupanda kuanzia 2004 hadi 2009.

Ukimya huu katika ndoa au uhusiano, ipo siku utaleta madhara kama vifo, ulemavu na uharibifu mkubwa. Kaka, baba zangu simameni…pazeni sauti zenu, wekeni wazi yanayowasibu ili Tanzania ibadili mtazamo wa unyanyasaji wa kijinsia.

Post a Comment

POPULAR POST

 
Top